Hapa ilikuwa wakati Kapalamya alipokuwa akirejesha bendera.
Mmoja wa wana Chadema aliyejiunga CCM, Mbungu akieleza sababu za kujiunga na CCM
Kwa pamoja wanachama hao walikula kiapo baada ya kukabidhiwa kadi za CCM
Mmoja baada ya mwingine walipata fursa ya kusema.
Walishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya
Iringa kimeendelea na oparesheni yake ya “Ondoa Msigwa” kwa kuendelea kuvunja
baadhi ya ngome zake na za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) za Jimbo
la Iringa mjini.
Baada ya hivikaribuni kufanya mkutano
katika kata ya Kihesa na kujizolea wanachama lukuki kutoka Chadema wakiwemo
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (Iuco):
Jana chama hicho kimempokea aliyekuwa
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Iringa, Musa
Mbungu.
Wengine waliojitoa Chadema na kujiunga na
CCM katika mkutano uliofanya katika eneo la Mwagongo kata ya Ruaha ni pamoja na
Mwenyekiti wa Kata hiyo, Siuna Kapalampya.
Mbali na Kapalampya ambaye pia alikuwa
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema Wilaya ya Iringa, yumo pia Katibu wa
Kata hiyo Yohanes Michael na wanachama wengine saba.
Katika tukio hilo lililoonekana kuwanyong’onyeza
baadhi ya wana Chadema waliokuwepo katika mkutano huo, kadi 47, bendera,
Katiba, Ilani na vitabu kadhaa vya miongozi ya chama hicho vilikabidhiwa kwa
Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Hassan Mtenga anayeelezwa kuwa mwiba usiovunjika
kwa Chadema.
Haikuelezwa mara moja kadi na vifaa
vingine vya chama hicho vitapelekwa wapi baada ya hapo lakini mmoja wa wana CCM
alisema “ruksa kwa Chadema kuja na kuchukua takataka zao.”
Katika taarifa yake ya jumla kwa mamia ya
wananchi waliohudhuria mkutano huo, Mtenga alisema; “safari ya Msigwa imeiva.” Huku
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati akiwasihi wananchi kuachana
na Chadema, chama alichokifananisha na tangazo linalopiga vita maambukizi ya
Virusi vya Ukimwi linalowasihi watu kuachana na Michepuko.
“Chadema ni mchepuko, mwaka 2010 tulikuwa
na hasira tukamchagua Mchungaji Msigwa kuwa mbunge, ombi langu kwenu rudini
Njia Kuu ambayo ni CCM, mkataeni Msigwa kwasababu anapinga maendeleo ya jimbo
hili na ndio maana kila Bajeti inayotengwa kwa maendeleo ya jimbo huwa
anaikataa” Kabati alisema.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya
CCM, Mahamudu Madenge kwa upande wake aliwataka vijana wanaoendelea kuishabikia
Chadema kutumia akili zao kutafakari kwa kina maamuzi yao hayo.
“Kuweni mashabiki wa maendeleo, fanyeni
kazi, msikae vijiweni na kulaumu serikali. Jiulizeni toka mmekuwa Chadema mmepata
nini iwe kutoka kwa wabunge wa Chadema au chama chao,” alisema.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa,
Amani Mwindi alipigilia msumari wa moto pale alipotoa taarifa ndefu ya
utekelezaji wa Ilani ya CCM tangu mwaka 2000 na akashangaa baadhi ya watu
wanaonufaika na utekelezaji huo akiwemo Mbunge huyo kuwatukana.
Mmoja wa wana Chadema aliyejiunga na CCM,
Mbungu alisema; “nachofahamu mimi ni kwamba Mchungaji Msigwa aliazimwa suruali
na CCM, lakini baada ya kuipata anajigamba kainunua mwenyewe, tumekaa Chadema
na tunajua hakuna kitu, kwahiyo tunamtaka ajiandae kununua suruali kwa gharama
zake katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.”
Mbungu alisema hawatalala, watapita
nyumba kwa nyumba, uvungu kwa uvungu ili kumshawishi kila mpiga kura kuichagua
CCM kwa kuoanisha sababu za kufanya hivyo na mapungufu yaliyoko Chadema na
mbunge wao.
Naye Kapalamya alisema; “najuta kupoteza
muda wangu kwa muda mrefu ndani ya Chadema, kwani mbali na chama hicho
kutukamua wanachama masikini ili tukichangie, hatujawahi kuona fedha
zinazopatikana na zile zinazotokana na michango na ruzuku zinavyorudi katika
ngazi ya chini ili zitumike kuimarisha chama.”
Alisema wanafahamu tabia ya baadhi ya
wana Chadema waliowaacha katika chama hicho kwamba watakuja na uzushi kuwa
tuliojitoa kwao na kujiunga na CCM tumenunuliwa.
Huo ni uongo na uzushi, wanachotakiwa
kujua ni kwamba hakuna mazingira mazuri ya siasa katika chama chao,
kinachoamuliwa na kufanywa na baadhi ya wakubwa hakipingwi, ukosefu wa
demokrasia hiyo ndio unaowakimbiza.
Katika mikutano iliyofanya katika kata zote 16 za jimbo la Iringa Mjini, CCM imejipatia wanachama 2,890, kabla ya kupata wanachama hao wapya CCM Iringa Mjini kwa mujibu wa Mtenga ilikuwa na wanachama zaidi ya 26,000.
Post a Comment