Dada mkuu wa wa shule Neema Mtisi akizungumza na wanahabari kuhusu namna wanavyoathirika kielimu.

Kwa muda wa siku mbili  walimu katika shule ya sekondari ya Kihesa iliyopo manispaa ya Iringa wameendesha mgomo wa kutoingia madarasani  kufundisha wakimshinikiza Afisa elimu taaluma manispaa  ya iringa kufika shuleni hapo na kumuondoa mwanafunzi aliyefukuzwa shule kwa makosa ya utomvu wa nidhamu.

Mwanafunzi huyo Lomina Chengula kidato cha pili D akiwa na wenzake mapema mwezi huu alisimamishwa masomo na uongozi wa bodi ya shule hiyo kwa makosa yasiyovumilika, lakini kioja kimejitokeza pale Afisa elimu taaluma huyo kuchukua jukumu la kumrejesha shuleni mwanafunzi huyo kinguvu.

Akisimulia kisa hiki mmoja wa walimu shuleni hapo ambaye amezungumza na ebony fm, pamoja na kuendelea na msimamo wa kutoingia darasani ameutaka uongozi wa juu akiwemo mkuu wa mkoa kuingilia suala hili kisheria na kuchukua hatua stahiki kwa kulinda maadili ya kazi ya ualimu.

Kwa mujibu wa malalamiko ya walimu hao ni juu ya ukubwa wa makosa yanayomkabili mwanafunzi huyu ambaye kwa taratibu hayawezi kuvumilika katika taasisi yoyote ya elimu nchini kutokana na baadhi ya makosa kuingilia maslahi na usalama wa familia za jamii inayowazunguka.

Kwa pamoja walimu hao wameshikilia msimamo wao wakidai kudhalilishwa na maamuzi ya kiongozi huyo huku wengine wakijenga hoja juu ya uhalali wa Afisa huyo kushika madaraka kutokana na rekodi mbaya ya uongozi aliyokuwa nayo tangu awali .

Kwa upande wa uongozi wa serikali ya wanafunzi ramani ya ulimwengu imezungumza na dada mkuu wa shule hiyo ambaye amedai kuwa maamuzi ya bodi yalikuwa sahihi na kwa muda huo kama viongozi walikuwa kwenye pilika za kumwandikia barua mkuu wa mkoa kufikisha kilio cha kukosa masomo kwa siku mbili mfululizo.

Juhudi za kumtafuta Afisa huyo ili kuthibitisha sakata hilo  ziligonga mwamba ,na kuamua  kumtafuta mkurugenzi wa manispaa ya Iringa ambaye kwa muda huo alikuwa safarini kikazi lakini bado jitihada za kuwapata viongozi ili kufahamu undani wa suala hili zinaendelea.

Post a Comment

 
Top