Mtenga akipokea kadi kutoka kwa mmoja kati ya wana Chadema wengi waliorudisha kadi na kujiunga na CCM
 Mwakalebela alisisitiza umoja ili kuing'oa Chadema katika uchaguzi ujao
 Madenge akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM


 Vijana wa Chuo Kikuu Iringa wakionesha kadi za CCM walizokabidhiwa.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetuma ujumbe mzito wa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kikimtaka ajiandae kuwa mkulima kwa kuwa sababu za kisiasa zilisababisha wapoteze jimbo hilo mwaka 2010 hazitarudiwa tena katika uchaguzi huo wa mwakani.
Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kihesa Sokoni mjini Iringa juzi, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Hassan Mtenga alisema; "tunamsihi azipoteze fedha zake bure  katika uchaguzi mkuu wa 2015, tutamshinda kweupe na hakutakuwa na lugha waliyozea ya wizi wa kura."

Alimtaka apokee ushauri wa bure ili yaliyowakuta wanasiasa wengine waliopata fursa ya kushauriwa na wakapuuza yasimkute yeye.
“Tuna muhakikishia Mchungaji Msigwa kwamba katika Uchaguzi wa 2015 hatutarudia kosa lililompa ushindi mwaka 2010,” alisema.
CCM ililaumiwa kupoteza jimbo hilo baada ya kufanya kosa la kiufundi kwa kuengua jina la aliyekuwa mshindi wa kura zake za maoni Frederick Mwakalebala na kumsimamisha aliyekuwa mshindi wa pili wa kura hizo, Monica Mbega.
Pamoja na chama hicho kutetea uamuzi wa kumuengua Mwakalebala na kumsimamisha Mbega aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kati ya mwaka 2000 na 2010, wafuasi na wanachama wengi wa CCM walitamka hadharani na kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwamba hawatampa kura zao Mbega.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayewakilisha Manispaa ya Iringa, Mahamudu Madenge alisema “kwa kuwa CCM ina tanuru la viongozi wenye uvumilivu, busara na hekima iwe iwavyo itaendelea kuongoza taifa hili kwa miaka mingi ijayo.”
Alisema CCM itatumia demokrasia yake kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi huo na ni imani yao kwamba wagombea wengine wote watamuunga mkono atakayeteuliwa.
“Miaka minne kwetu sisi tunahesabu kama miaka ya mateso; na tuna mwaka mwingine wa kumalizia mateso toka kwa mbunge wa upinzani, hakika 2015 inatakiwa kuwa mwisho,” alisema.
Alisema pamoja na kupinga bajeti zote tangu awe mwakilishi wa jimbo hilo la Iringa Mjini, mbunge huyo amekuwa akirudi kinyemela na kuwadanganya wapiga kura kwamba kazi zinazofanywa na serikali ya CCM zinafanywa na yeye.
Kwanini CCM inajinasibu kila uchao kuchukua jimbo hilo?
1. Ni kile wanachoeleza mafanikio makubwa wanayopata katika kutekeleza Ilani yao ya uchaguzi
2. Migogoro ya kisiasa na kiuongozi inayoisibu Chadema Iringa Mjini. Moja ya mgogoro huo unamuhusisha Msigwa kama mbunge wa jimbo hilo na Chiku Abwao kama mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa. Kwa miaka zaidi ya mitatu wawili hao wanasemakana hawapikiki chungu kimoja.
3. Ni hazina ya watu wenye uwezo iliyonayo CCM wakati ikijipanga kuelekea katika uchaguzi huo.

Viongozi wanaotajwatajwa kufaa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Mahamudu Madenge, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Viti Maalumu Ritta Kabati, Fredrick Mwakalebela, Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Population Service International, Romanus Mtung’e na Daktari wa magonjwa ya wanawake na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Dk Yahaya Msigwa.
Wengine ni pamoja na mwanamichezo maarufu nchini anayetoka kundi la marafiki wa Simba, Zakaria Hanspope na aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Fadhil Ngajiro.

Post a Comment

 
Top