Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa imetahadharisha juu ya ongezeko la idadi ya watu wanaolazimika kuzihama nyumba zao huko Sudan Kusini, huku kukitarajiwa kuweko na ongezeko jingine la wakimbizi wengine laki saba ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza na vyombo vya habari hapo jana, Melissa Fleming msemaji wa UNHCR amesema hali ya kibinadamu ni mbaya huko Sudan Kusini kutokana na kuibuka mapigano kati ya vikosi vya serikali na vya waasi wa nchi hiyo.

Fleiming ameongeza kuwa mgogoro unaoendelea katika nchi hiyo changa zaidi duniani unachochea wimbi kubwa la wakimbizi wa nchi hiyo kwenda kutafuta hifadhi katika nchi za Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda, idadi ambayo amesema ni kubwa kuliko ile iliyotarajiwa.

Wakati huohuo shirika la UNHCR limeomba msaada wa dola milioni 658 kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi wa Sudan Kusini.
BBC-Swahili 

Post a Comment

 
Top