Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa majaribio ya kitiba ya chanjo za virusi vya ugonjwa wa ebola yataanza muda si mrefu na kwamba njia za kitiba za kujilinda na maradhi hayo zitapatikana mapema mwakani. Marie-Paule Kieny Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani amesema kwamba ni kweli kuwa chanjo ya ugonjwa wa ebola itaanza kufanyiwa majaribio karibuni hivi na kuwa tayari kutumiwa mwakani.

Hadi sasa hakuna tiba kwa ajili ya ugonjwa hatari wa ebola ambao huambatana na mgonjwa kuwa na homa kali huku akitapika, kuhara na kuvuja damu. Karibu watu 1000 wameshaaga dunia kutokana na homa ya ebola tangu ugonjwa huo hatari uliporipuka magharibi mwa Afrika mwezi Machi mwaka huu. Jean-Marie Okweo Bele mkuu wa chanjo katika Shirika la Afya Duniani amesema kuwa kampuni ya madawa ya Uingereza ya Glaxo Smith Kline inakadiria kuanza majaribio ya chanjo ya ebola mwezi Septemba mwaka huu na kwamba kuna uwezekano mkubwa chanjo hiyo ikawa tayari mwaka 2015.

Post a Comment

 
Top