Watu wanane wamekufa papo hapo, wengine
tisa kujeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi baada ya
gari aina ya Land Rover, mali ya Halmashauri ya Mji Masasi kupata ajali katika
kijiji cha Mtama wilaya ya Lindi Vijijini mkoani humo.
Gari hilo lenye namba za usajili STL 1615,
lilikuwa linatokea Lindi ambako maofisa wa Halmashauri ya Masasi walikuwa
wanashiriki katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika kitaifa
katika Viwanja vya Ngongo, nje kidogo ya Manispaa ya Lindi.
Kutokea kwa ajali hiyo kulithibitishwa mwishoni mwa wiki iliyopita na
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga aliyesema ilitokea juzi
majira ya saa 11.30 jioni katika kijiji cha Mtama.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Issa Salumu (33),
Malik Selemani (24), Juma Ausi (21), Rajab Khalfan (17), Said Mchora (24) na
Fadhili Mchalasi (26) ambapo watu wawili hadi sasa hawajafahamika majina yao,
na amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi. Marehemu wote ni wakazi wa
kijiji cha Mtama.
Kwa mujibu wa Kamanda Mzinga, waliojeruhiwa kwenye
ajali hiyo ni dereva wa gari hilo, Kessy Mwaijande (40). Pia wamo madiwani
watano wa Halmashauri ya Mji Masasi ambao ni Habiba Amlima, Maimuna Chiputa,
Exaveria Mhagama, Asha Abbas na Blandina Nakajumo.
Wengine ni Abraham Mohammed, Shaabani Issa Kitemwe
na Ally Adam, wote wakazi wa kijiji cha Mtama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashuhuda wa
ajali hiyo walisema kuwa majira ya jioni kwenye eneo hilo la tukio, waliliona
gari hilo likiwa kwenye mwendo kasi, mazingira ambayo yalisababisha dereva wa
gari hilo aliyekuwa akijaribu kukwepa mbuzi waliokuwa barabarani kushindwa kumiliki
gari hilo na hatimaye kuacha njia na kuwagonga watu waliokuwa pembezoni mwa
barabara hiyo, waliokuwa wakifanya biashara ndogo.
Hata hivyo, mmoja wa mashuhuda hao, Ahmad Mbonde
alimwambia mwandishi kuwa, kama si kuwakwepa mbuzi, dereva wa gari hilo asingesababisha
ajali.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Mzinga amewataka
madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kunusuru maisha ya watu
wanaoendelea kupoteza maisha na huku wengine wakibaki na ulemavu,
mazingira ambayo hupunguza nguvu kazi ya Taifa.
Post a Comment