ALIYETAKA kumzika mtoto wake akiwa hai
baada ya ng’ombe wao aliyekuwa akimchunga kuliwa na mamba alipopelekwa kunywa maji
katika Mto Ruvuma, anashikiliwa na Polisi baada ya kukamatwa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni
Tundu Jilala (40) mkazi wa kijiji cha Nambendo kata ya Muhukuru wilayani
Songea.
Alisema Septemba 5, mwaka huu, majira saa
8.00 mchana, Jilala alifanya ukatili kwa mwanaye huyo mwenye umri wa miaka 11
(jina linahifadhiwa) baada ya kusudio lake la awali la kumtumbukiza katika mto
huo ili naye aliwe na mamba kutofanikiwa.
Kabla ya kutaka kumzika akiwa hai, Jilala
kwa kile kilichoelezwa alikasirishwa baada ya ng’ombe wake kuliwa na mamba
wakati akichungwa na mwanaye huyo, aliamua kumtumbukiza katika mto huo ili mtoto huyo naye aliwe.
Hata
hivyo kusudio hilo alikuza matunda kwani mtoto huyo alinusurika baada ya kusukumwa na maji hayo hadi ng’ambo ya
pili ya mto.
Baada
ya kunusurika, mtoto huyo aliyejificha porini kesho yake alipata akili
ya kwenda kwa mtendaji wa kijiji hicho na kuomba msaada.
“Mtendaji huyo alikwenda na mtoto huyo hadi
nyumbani kwao na alipofika walikuta umati wa watu wakiwa kwenye matanga
aliyokuwa ameyaandaa baba yake mzazi kwa imani kwamba mwanaye huyo amekufa
baada ya kuliwa na mamba, RPC huyo alisema.
Baada ya Jilala kumuona mtoto wake akiwa
hai alichanganyikiwa na baada ya watu kutawanyika aliongea na mdogo wake
aliyetajwa kwa jina la Sokoma Jilala waliyekubaliana wachimbe shimo kubwa kisha
wamzike akiwa hai.
Bahati iliendelea kuwa ya mtoto huyo
kwani alifanikiwa kuchoropoka kabla hajatumbukizwa katika shimo hilo ili afukiwe.
Mtoto huyo inaelezwa kwamba alirudi tena
kwa afisa mtendaji wa kijiji ambako alimkuta pia afisa tarafa ya Muhukuru,
Salma Mapunda na baada ya kuwasilimua mkasa mzima walimchukua hadi kituo kikuu
cha Polisi cha Songea mjini.
Msikhela alisema jeshi la Polisi
limefanikiwa kumkamata baba mzazi wa mtoto huyo huku mdogo wake Sokoma Jilala akiendelea
kutafutwa baada ya kutokomea kusikojulikana.
Post a Comment