Wakati wanafunzi wa shule za msingi wanatarajia kuanza kufanya mtihani wa kuhitimu elimu hiyo kesho nchini kote; Ebeneza Mtivike  wa shule ya msingi Ikelu iliyoko katika Halmashauri ya Mji Makambako atafanya mtihani huo akiwa amelala kwenye godoro.
Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji Makambako, Shomari Bane alisema Mtivike atafanya mtihani huo katika mazingira hayo shuleni hapo kwasababu ni mgonjwa wa muda mrefu asiye na uwezo wa kukaa kwenye dawati.
Alisema ili kumtendea haki mwanafunzi huyo, ataongezewa muda kwa baadhi ya mitihani.
Watakapokuwa wanafanya mtihani wa hisabati mwanafunzi huyo ataongezewa dakika 10 huku masomo mengine ya Sayansi, Kingereza na Maarifa ya Jamii ataongezewa dakika 15.
Kwa mujibu wa taarifa ilitotolewa na Afisa Elimu Mkoa wa Njombe, Said Nyasiro mwanafunzi huyo atafanya mtihani huo akiwa amelazwa kwenye godoro kwasababu anaugua ugonjwa wa kichocho kwa muda mrefu.
Nyasiro alisema mwanafunzi huyo ataungana na watahiniwa wengine 17,300 wa mkoa mzima wa Njombe kufanya mtihani huo.
Kati ya watahiniwa hao, alisema wapo wawili wasioona wa wilaya ya Wanging’ombe na walemavu wa ngozi 22.
Alisema mkoa wa Njombe una matarajio makubwa kwamba kiwango cha ufaulu kitaongezeka mwaka huu kutoka asilimia 70.7 za watihani uliopita.


Post a Comment

 
Top