Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameamuru mabango ya hekeheka za uchaguzi yenye nembo ya kauli mbiu ya 'Bring Back Jonathan 2015' yang'olewe mara moja.

Mabango hayo yamelaaniwa vikali kwenye mitandao ya kijamii kwani yanaonekana kuiga kauli mbiu iliyotumiwa katika kampeini ya kuitaka serikali kuwaokoa wasichana waliotekwa nyara na wanamgambo wa Boko Haram mwezi Aprili mwaka huu.

Kundi hilo la wapiganaji wa kiisilamu bado linawashikilia wasichana hao, Wakati ambapo mabango ya Bring Back Jonathan 2015 yaliowekwa kando ya barabara kuu mjini Abuja, yalilaaniwan vikali nchini Nigeria na kimataifa kupitia katika mitandao ya kijamii.

Watu walihisi kuwa ilikuwa ni kama kejeli kwa kampeini ya 'Bring Back Our Girls' ambayo ilienea kote duniani baada ya Boko Haram kuwateka nyara wasichana wa shule ya Chibok.

Wasichana hao 219, bado hawajulikani waliko miezi mitano baada ya kutekwa kwao.
Rais Jonathan, ameyataka mabango hayo kuondolewa kwenye barabara za mji haraka iwezekanavyo.

Katika taarifa yake alisema yeye pamoja na wanigeria wengi wanahisi kuwa kampeini hiyo ilikuwa na nia mbaya na kusisitiza kuwa juhudi bado zinafanywa kuwoakoa wasichana hao waliotekwa na Boko Haram.

Post a Comment

 
Top