ASKOFU
Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela amesema haoni
shida nchi ikipata rais kijana wakati akizungumzia sifa za rais ajaye.
Kati
ya wagombea lukuki walioonesha nia ya kuwania nafasi hiyo, vijana pekee waliotangaza
kuwania nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani ni Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari Makamba kutoka Chama cha Mapinduzi
(CCM).
Na
kwa upande wa vyama vya upinzani, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(Chadema), Agosti mwaka huu alifunguka na kusema ana nia ya kuwani urais katika
Uchaguzi Mkuu wa 2015 iwapo chama chake kitaridhia.
Alitoa
kauli hiyo ikiwa ni miaka miwili tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
(Chadema) alipojitokeza hadharani akisema kwamba hatawania tena ubunge katika
jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu ujao na badala yake atajitosa kwenye urais.
Akizungumza
na wanahabari mjini Mafinga juzi, Askofu Mtetemela alisema; “kwangu mimi umri
sio hoja hata kidogo, yoyote anaweza kuwa rais, awe kijana au mzee sina shida,
lakini mbali na sifa nyingine zinazotajwa ni lazima awe na sifa kuu mbili kwa
mtazamo wangu,” alisema.
Akizitaja
sifa hizo, alisema Rais ajaye ni lazima awe mwadilifu anayepimika kwa matendo
na maneno yake lakini pia ni lazima awe na moyo wa mabadiliko kwa watu wake
akiunga mkono juhudi za waliomtangulia katika kuwakwamua watanzania na
umasikini.
Akizungumzia
tuhuma zinazorushwa dhidi yake kwamba maoni yake katika bunge la katiba
yanamuondolea sifa ya kuwa mwakilishi anayetoka katika taasisi za dini, Askofu
Mtetemela alisema yeye sio mwanachama wa chama chochote cha siasa nchini na
kwamba wanaomuhusisha na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwasababu ya msimamo wake
katika mchakato wa Katiba Mpya wanakosea.
“Niko
katika bunge maalumu la katiba nikiwawakilisha waumini wangu, wenye itikadi
tofauti. Nikiwa chama fulani sitawatendea haki lakini naitwa CCM kwasababu ya
msimamo wangu,” alisema alipokuwa akizungumza na wanahabari juzi, mjini
Mafinga.
Pamoja
na kujinasibu hivyo, tamko la Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) lililochapishwa
kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya jana, limewakana wachungaji na maaskofu
walio ndani ya bunge hilo (akiwemo Askofu Mtetemela) wanaodai kuteuliwa na
kuwakilisha taasisi za dini.
Katika
tamko lake hilo, CCT imesema ilipeleka wajumbe tisa ambao kati yao mjumbe mmoja
tia ambaye ni Esther Msambazi ndiye aliyeteuliwa.
“Viongozi
wengine wa dini ya kikristo (maaskofu na wachungaji) waliopo katika bunge hilo
hawakutumwa na CCT na wala CCT haina taarifa ni vipi walichaguliwa kuwa wajumbe
wabunge maalumu la Katiba,” lilieleza tamko hilo
Askofu
Mtetemela alisema anarushiwa madongo hayo na watu waliotaka awe upande wao na
asiendelee kushiriki katika bunge hilo ili kuwafurahisha.
“Siwezi
kutoka kwasababu ya kuwafurahisha watu fulani. Bunge linaendelea kisheria na
akidi ya vikao vyake inaruhusu. Kwanini nitoke?” alisema.
Alisema
yeye ni mmoja wa wajumbe wa bunge hilo wanaounda kundi la 201 ambao kimsingi
wanawakilisha makundi tofauti ya jamii na sio vyama vya siasa ambavyo tayari
vinawawakilishi wake ambao ni wabunge.
Akizungumzia
maoni yanayotolewa na baadhi ya taasisi za dini kuhusu kusitishwa kwa mchakato
huo mpaka yatakapopatikana maridhiano ya
pande zinazosigana;
Askofu
Mtetemela alisema taarifa potofu wanazopata kutoka katika vyanzo visivyo sahihi
zimepelekea yatolewe matamko yanayotaka kuhatarisha mchakato huo.
“Kuna
mambo yanatokea nje ya bunge na yanaoonekana yana nguvu kwa wananchi lakini
ukweli wa mambo huko ndani ya bunge. Tunaijadili rasimu na si vinginevyo, pale
tunapoona pako sawa hatuna shida lakini yapo maeneo ambayo yanahitaji
kuboreshwa na hiyo ndio kazi tunayofanya kwasababu maana ya bunge maalumu la
katiba sio kukubali kila kitu kilicholetwa kwenye rasimu” alisema.
Alisema
kinachofanywa na bunge hilo sio hitimisho la watanzania kupata katiba mpya na
ni makosa kuwahukumu hivisasa kwani baada ya kazi yao, katiba hiyo itapelekwa
mbele yao ili ipigiwe kura.
Post a Comment