Zoezi la kuonesha mipaka ya wawekezaji hao lifanywa.
Diwani wa kata ya Idodi, Onesmo Mtatifikolo akieleza jambo katika tukio hilo.
WANANCHI wa kata ya Idodi wilayani Iringa wameituhumu kampuni ya Kilombero North Safaris kuingia katika mipaka ya uwekezaji isiyomuhusu na kuwabugudhi wawekezaji wengine.
Idodi
ni moja kati ya vijiji 21 vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Malihai Tarafa ya
Idodi na Pawaga (Mbomipa) inayopokana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Mwenyekiti
wa Mbomipa Phillip Mkumbata amenukuliwa
mara kadhaa akithibitisha kwamba kampuni ya Kilombero North Safaris, miaka
micheche iliyopita iliingia mkataba na jumuiya hiyo wa kuwekeza katika eneo
lenye ukubwa wa kilomita za mraba 2 katika kanda ya uwekezaji ya Lunda kwa
ajili ya kujenga kambi na hoteli za kitalii.
Katika
mazingira yaliyopata kuelezwa na Diwani wa Kata ya Ilolompya, Fundi Mihayo
kwamba ni ya kutatanisha, mwaka 2012 wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya
Iringa na wizara ya Maliasili na Utalii waliilazimisha jumuiya hiyo kuingia
mkataba wa miaka 25 na kampuni hiyo, mkataba unaopingwa na wananchi wanaounda
jumuiya hiyo.
Katika
tukio la hivikaribuni na ambalo limewakasilisha wananchi wa kijiji cha Idodi
mwekezaji huyo aliingia katika eneo la Ilusi lililotolewa kwa kampuni nyingine
ya Mkwawa Hunting Safaris Ltd kwa shughuli za uwindaji na ujenzi wa hoteli.
Septemba
5, mwaka huu, wafanyakazi watano wa Kilombero North Safaris waliingia katika
eneo la Ilusi lililotolewa na kijiji cha Idodi kwa kampuni ya Mkwawa hunting
Safaris na kuwakamata wageni watatu toka nchini Italia waliokuwa wakitalii na
kuwinda katika eneo hilo.
Mmoja
wa wafanyakazi wa Kilombero North Safaris, Charles Gwero alisema waliwakamata
wageni hao na kuwanyang’anya leseni za uwindaji wakiamini kwamba eneo la Ilusi
lipo ndani ya mipaka ya kampuni yao.
“Tuliwakamata
wageni hao kwakuwa tulikuwa hatujui vizuri mwisho wa mipaka yetu; walipokuja
wana vijiji na kutuelewesha tukawarudishia leseni zao na kufikia muafaka wa
mgogoro huo,” alisema.
Kaimu
Mkurugenzi wa Mkwawa Hunting Safaris Ltd, Mohamed Huwel alisema; “kitendo
kilichofanywa na kampuni ya Kilombero ni cha kusikitisha kwani kinaonekana
kilifanywa kwa lengo la kuchafua jina la kampuni yetu.”
Huwel
alisema kampuni yao itakutana na mwanasheria wao ili waangalie uwekezano wa
kuishitaki kampuni ya Kilombero kwa kuwadhalilisha wageni wao waliokasilishwa
na tukio hilo.
Diwani
wa kata ya Idodi, Onesmo Mtatifikolo aliishutumu kampuni ya Kilombero akisema kitendo
ilichofanya dhidi ya mwekezaji mwingine katika eneo hilo kinalenga kuigombanisha
Mbomipa na mwekezaji huyo.
“Sio
kweli kwamba hawajui mipaka yao, tunaamini wanaijua vizuri; lakini walifanya
kusudi ili kuiharibia kampuni ya Mkwawa na mwishowe Mbomipa,” alisema.
Katibu
wa Maliasili wa kijiji cha Idodi, Dani Salumo alisema wafanyakazi wa Kilombero
North Safaris wamekuwa na kawaida ya kuingia katika maeneo mengine katika eneo
la hifadhi ya jumuiya hiyo bila taarifa.
Mwenyekiti
wa kijiji cha Idodi, Musa Kigohelo aliiomba serikali kuingilia kati mgogoro wa
uwekezaji unaoendelea baina yao na kampuni hiyo ya Kilombero.
Mgogoro
huo kwa mujibu wa Afisa Wanyamapori wilaya ya Iringa, Rachel Nhambu
umesababisha kwa muda sasa kampuni hiyo isiilipe Mbomipa ada zake za uwekezaji
na hivyo kuipotezea mapato makubwa.
“Ni jambo la kusikitisha wanaingia katika eneo
la mtu mwingine na kuwabugudhi wahusika. Hata kama tuna mgogoro nao, ni lazima
wafuate taratibu ili Mbomipa na vijiji vyake visikose mapato toka kwa
wawekezaji wengine” alisema Mwenyekiti wa kijiji.
Post a Comment