MWANAHABARI Frank Kibiki, aliyewahi kuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) ngazi ya wilaya kwa zaidi ya miaka 10, ametangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Kibiki ambaye ni mume wa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Tumaini Msowoya ametangaza nia hiyo juzi kupitia kituo cha redio cha Overcomers FM cha mjini Iringa.
Kibiki aliyepata kuwa Katibu wa UVCCM Iringa Mjini, ameishia kutangaza nia akisema hawezi kusema mengi kwasasa kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kufanya kampeni jambo ambalo kwa mujibu wa kanuni za CCM ni kosa.
Kwa kufanya hivyo Kibiki ambaye ni mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, anakuwa mwana CCM wa kwanza kutangaza nia hiyo huku wana CCM wengine wakiwatajataja baadhi ya makada wao wanaoona wanafaa kumenyana na Mbunge wa sasa wa jimbo hilo Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) kama naye atateuliwa tena na chama chake kuwania nafasi hiyo.
Wanaotajwa ni pamoja na Nuru Hepautwa, Jesca Msambatavangu, Mahamudu Madenge, Salim Asas, Dk Yahaya Msigwa, Frederick Mwakalebela, Zakaria Hanspope, Fadhili Ngajiro na Ritta Kabati.

Post a Comment

 
Top