Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Leopold Fungu akitoa taarifa ya matukio ya ajali mkoani Iringa.
 Taxi zilikuwepo kwenye maadhimisho hayo.
 Maandamano yaliongozwa na Brass Band ya JKT Mafinga.
 RPC Ramadhani Mungi alitoa ushauri wa nini kifanyike kupunguza ajali nchini
 Salim Asas akapongezwa kwa mchango wake katika kukisaidia kikosi cha usalama barabarani kutekeleza wajibu wake.
 Mstahiki Meya, Amani Mwamwindi akaelezea mikakati ya manispaa yake ya Iringa katika kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami.
 Kwaya ya shule itatoa ujumbe kwa madereva na watumiaji wa barabara.
 Kukawa na burudani toka kikundi cha Mkwawa Magic Centre, hapa mmoja wa vijana wanaounda kikundi hicho akishindana na nyani wake kunywa soda.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo.


TAXI zinazotoa huduma ya usafirishaji abiria mkoani Iringa, zimeelezwa na jeshi la Polisi kuwa ndio usafiri salama kuliko mwingine wowote mkoani hapa.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani mkoani Iringa inaonesha hakuna taxi hata moja iliyopata ajali na kusababisha vifo tangu Januari hadi Desemba mwaka huu.
Kamanda Mungi alivitaja vyombo vinavyoongoza kwa ajili na kusababisha vifo mkoani Iringa kuwa ni magari madogo binafsi, mengi yakiwa ni yale yanayopita katika barabara kuu ya Dar es Salaam Iringa Mbeya.
Alisema magari makubwa ya mizigo yanashika nafasi ya pili kwa ajali zinazosababisha vifo mkoani hapa, yakifuatiwa na pikipiki (bodaboda) na mabasi makubwa na yale madogo (daladala) yanayotoa huduma ya usafirishaji abiria katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa.
Mungi alisema lengo la mkoa wa Iringa kwa mwaka huu lilikuwa kupunguza ajali kwa asilimia 20 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2, kutoka asilimia 18 za mwaka jana.
Alisema ajali zinazoendelea kutokea maeneo mbalimbali nchini haziwezi kumalizwa kwa oparesheni bali ni kwa kuboresha sera na mikakati iliyopo kwa kuhusisha wizara mbalimbali zinazohusika na ajali zinazotokana na vyombo vya usafiri.
Alizitaja wizara hizo kuwa ni pamoja na wizara ya mambo ya ndani, ujenzi, uchukuzi, fedha, nishati na madini, biashara na viwanda, Tamisemi, afya, sheria na katiba na wizara ya kazi na ajira.
Awali Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Iringa, Leopold Fungu alisema ajali za barabarani zimekuwa zikisababishwa na ubovu wa magari, makosa ya kibinadamu na kutofuatwa kwa sheria na kanuni za usalama barabarani.
“Ajali nyingi zinatokea kwasababu ya mwendo kasi, uzembe wa utumiaji barabara, tatizo la kutojua kanuni na sheria za usalama barabarani, ulevi na nyasi ndefu kando ya barabara, ” alisema.
Katika kukabiliana na ajali mkoani hapa, Fungu alisema uwekaji matuta na alama za barabarani unaendelea kuimarishwa sambamba na ukamataji wa magari kwa kutumia vipima mwendo, kukagua magari ya abiria na mizigo, kupima madereva walevi na kuondoa magari mabovu barabarani.
Akizungumzia takwimu za makosa ya usalama barabarani katika kipindi cha miezi nane, mwaka jana na mwaka huu, Fungu alisema wakati mwaka jana kulikuwa na ajali 95, mwaka huu kuna ajali 116 hadi sasa.
Kuhusu ajali za vifo, alisema wakati mwaka jana zilikuwa 57 mwaka huu zimetokea 92, huku ajali za majeruhi zikipungua kutoka 28 hadi 24 mwaka huu.
Alisema wakati idadi ya watu waliofariki ikipungua kutoka watu 86 hadi 41, waliojeruhiwa wamepungua pia kutoka 59 hadi 58 zikiwa zimesalima siku chache kabla ya kufunga mwaka.
Kuhusu makosa ya kawaida, Fungu alisema tofauti na makosa ya 18,078 yaliyotokea mwaka jana, mwaka huu yameongezeka hadi 25,009.
Katika hafla hiyo ambayo mgeni wake rasmi alikuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi, Fungu alimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Asas kwa kukichangia kikosi cha usalama barabarani magari mawili na vipimia ulevi na mwendokasi 30.

Post a Comment

 
Top