RAIS Jakaya Kikwete, leo anatarajiwa kukata mzizi wa fitina kwa kutoa maamuzi juu ya mapendekezo nane yaliyowasilishwa kwake na Bunge, kutokana na sakata lililozua mtafaruku bungeni la akaunti ya Tegeta Escrow.
Anatarajiwa kuzungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam na kutoa kinagaubaga juu ya sakata hilo baada ya uamuzi wake kusubiriwa kwa hamu na wananchi kutokana na kuahirisha kutoa maamuzi yake juu ya mapendekezo hayo mara kadhaa.
Sakata hilo lililoibuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupitia ripoti ya uchunguzi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), liliibua hisia za wananchi wake hasa kutokana na moja ya maazimio hayo nane kupendekeza Rais Kikwete awachukulie hatua mawaziri na wateule wake wote waliohusishwa katika sakata hilo.
Mawaziri na wateule wa Rais Kikwete waliohusishwa katika sakata hilo ni pamoja na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Eliakim Maswi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema.
Tayari Werema ameandika barua ya kujiuzulu kutokana na sakata hilo la uchotwaji wa Sh bilioni 306 katika akaunti hiyo ya Tegeta Escrow na Rais Kikwete amesharidhia ombi la mwanasheria huyo kujiuzulu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete leo anatarajiwa kuzungumza na wazee hao wa Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo suala hilo la sakata la Escrow.
Katika taarifa hiyo ya Ikulu imebainisha kuwa Rais atazungumza na wazee kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa yakiwemo yale yanayosubiri uamuzi wake tangu alipokuwa akijiuguza baada ya kufanyiwa upasuaji Novemba, mwaka huu.
Mara baada ya kurejea kutoka nchini Marekani, alikokwenda kutibiwa, alikiri kupokea maazimio hayo na kuagiza ripoti ya CAG iwekwe hadharani na kutangazwa katika vyombo vya habari ili kila mwananchi aisome na kuielewa.
Katika ripoti hiyo ya CAG ilibainisha mapendekezo ya kufanyiwa kazi na Serikali ambayo ni pamoja na kufanywa kwa uchunguzi na vyombo husika kuhusu miamala ya malipo iliyotokea Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na akaunti za Pan Africa Power Solutions (T) ili kubaini uhalali na usahihi wake.
Aidha ilipendekeza BoT ifanye uchambuzi wa gharama ilizotumia wakati wa kutekeleza wajibu wake kama wakala wa uendeshaji wa akaunti hiyo pamoja na zile za kisheria ili iweze kufidiwa na wahusika.
Pendekezo lingine la ofisi ya CAG katika ripoti hiyo ni kuhusu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchukua hatua stahiki kuhakikisha Serikali na BoT zinakingwa dhidi ya madai yoyote yanayoweza kujitokeza kwa kutumia kinga iliyotolewa na IPTL.
Pia lipo pendekezo katika ripoti hiyo linalotaka Serikali kufanyia uchunguzi miamala ya mauzo ya hisa kutoka kampuni zilizokuwa zikimiliki IPTL kwenda PAP na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kufuatilia kodi kuhusu mauzo na hisa hizo.
Wakati ripoti hiyo ikitoa mapendekezo hayo, baada ya sakata hilo kuwasilishwa bungeni na kuchafua hali ya hewa, Bunge nalo liliibuka na maazimio yake ambayo ni pamoja na kumtaka Rais Kikwete kuwawajibisha baadhi ya mawaziri na watendaji wakuu waliohusishwa katika sakata hilo.
Pia Bunge hilo liliazimia kuundwa tume ya majaji kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za utobu wa maadili dhidi ya Majaji Aloysius Mujulizi na Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu Tanzania ambao wanatuhumiwa kukiuka maadili hayo.
Pamoja na hayo Bunge hilo, pia liliazimia wenyeviti watatu wa Kamati za Kudumu za Bunge ambao ni Andrew Chenge, William Ngeleja na Victor Mwambalaswa wajipime wenyewe katika nyadhifa zao na kuachia ngazi.
Chenge ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Ngeleja ni Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na Mambalaswa ni Mwenyekiti katika Kamati ya Nishati na Madini.
Wakati Watanzania wakisubiri kwa hamu mkutano huo wa Rais Kikwete na wazee leo, tayari kampuni za Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP) na Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Harbinder Singh Sethi, wamefungua kesi ya kikatiba kupinga utekelezaji wa maazimio ya Bunge yaliyotolewa kuhusu sakata hilo la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kesi hiyo ilifunguliwa mwishoni mwa wiki katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati ya dharura dhidi ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ilifunguliwa kupitia mawakili watatu wa kampuni hizo, ambao ni Joseph Makandege, Melchsedeck Lutema na Gabriel Mnyele. Mawakili hao wanadai kwamba uamuzi uliotolewa na Bunge, uliegemea upande mmoja kwa vile baadhi ya wahusika walioshiriki, ikiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila wana kesi kuhusu sakata hilo.
Pia, walidai kilichofanyika ndani ya Bunge kuhusu sakata hilo ni kinyume cha Katiba kwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria alitafsiri vibaya amri halali, iliyotolewa na Mahakama ya kuzuia mjadala huo usijadiliwe bungeni.
Mawakili hao walidai kwamba Mahakama ilikusudia Bunge liweze kuendelea na shughuli zake za kawaida wakati shughuli nyingine zinazohusu maombi hayo zikitekelezwa.
Miongoni mwa maazimio yaliyowasilishwa bungeni ni kwamba Sethi, James Rugemalira, Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), walihusika kufanya miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kwenda kwa kampuni za PAP na VIP Engineering & Marketing.

Post a Comment

 
Top