Bernard Murunya.
Waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro akiwamo aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo ambaye kwa sasa
ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Bernard Murunya wamepandishwa kizimbani
jana katika Mahakama ya Wilaya ya Karatu kujibu tuhuma mbalimbali
zinazowakabili ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka wakati wakiwa watumishi
katika mamlaka hiyo.
Waliofikishwa mahakamani hapo ni
washtakiwa watano, mbali ya Murunya, wengine ni Leornard Minzi aliyekuwa Mkuu wa
Kitengo cha Ununuzi na Victor Appolo aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ikolojia.
Wengine ambao mpaka sasa ni watumishi
katika mamlaka hiyo ni Bruno Kawasange, Mkurugenzi wa Hifadhi na Maendeleo ya
Jamii na Justice Muumba, Meneja wa Maendeleo ya Jamii.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Ally Mkama, mwendesha mashtaka wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hamidu Sindano akishirikiana na
Richard Jacopiyo.
Waliieleza Mahakama kuwa katika tarehe
tofauti kati ya Aprili na Februari, 2011 na 2012, washtakiwa walitumia madaraka
yao vibaya kwa kushawishi kumpa kazi mtaalamu mshauri, Michel Duplat raia wa
Ufaransa bila kufuata utaratibu ulioelekezwa na Sheria za Ununuzi ya Umma
ya Mwaka 2004, kitendo kilichosababisha Duplat kulipwa fedha za umma kinyume na
utaratibu.
Washtakiwa kwa pamoja walikana mashtaka
yanayowakabili, hawakutakiwa kuzungumza chochote mahakamani hapo na waliachiwa
kwa dhamana na wakiamriwa kutosafiri nje ya nchi.
Kesi hiyo iliahirishwa na itatajwa tena
Januari 6, mwakani kwa kuendelea kusikilizwa.
chanzo;mwananchi.co.tz
Post a Comment