Tafrani ilizuka Dar es Salaam na mjini
Tunduru, mkoani Ruvuma, baada ya majambazi kuua mtu mmoja na kupora zaidi ya
Sh10 milioni katika matukio mawili tofauti.
Tukio la kwanza lilitokea jana katika
eneo la Morocco, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam ambako majambazi walipopora
Sh2 milioni kwa Nuru Patrick, huku mpita njia, Gloria Uroki akiuawa kwa risasi.
Majambazi hayo yakiwa na silaha,
yalipora mkoba wenye fedha na wakati wanataka kukimbia, walianza kurusha risasi
hovyo na kusababisha kifo cha Uroki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa
Kinondoni, Camillius Wambura alisema tukio hilo lilitokea saa kumi jioni.
“Majambazi hao inaelekea walifahamu
kuwa mwanamke huyo ana fedha, kwa sababu aliposhuka tu kwenye daladala
walimvamia na kumpora mkoba,” alisema Wambura.
Katika tukio la Songea, watu wanaodaiwa
kuwa ni majambazi waliokuwa na bunduki aina ya SMG walimpora mfanyabiashara wa
madini raia wa Sri Lanka, Fadhiri Faiz (24) Sh8 milioni na simu tatu za
mkononi zenye thamani ya Sh1.8 milioni akiwa nyumbani kwake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo
Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 1.40 usiku katika Mtaa wa
Misufini, Kata ya Mlingotini wilayani Tunduru.
Alisema kabla ya uporaji, majambazi hao
walifyatua risasi nne hewani na kumteka mlinzi wa Kampuni ya Wan Security,
Hassan Silaji (40), kisha wakavamia nyumbani kwa mfanyabiashara huyo.
Post a Comment