Mtoto Nasra baada ya kutolewa kwenye box.



Wakazi wawili wa mtaa wa Azimio katika kata ya Kiwanja cha ndege Mkoani Morogoro wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumfanyia ukatili mtoto mwenye anayefahamika kwa jina la Nasra Rashid umri wa miaka minne na miezi sita ambaye inadaiwa kwa zaidi ya miaka mitatu mtoto huyo alifungiwa ndani ya boksi kama mnyama, ili asimuambukize mama mlezi virusi vya Ukimwi.

Watuhumiwa hao ambao ni Mariam saidi na mumewe Mtonga Omari wamekamatwa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na idara ya ustawi wa jamii baada ya kupata taarifa kutoka kwa majirani ambao waliling’amua hilo na kushindwa kuvumilia unyama huo.



Unyama huo wa kusikitisha, umefanyika muda wote huo bila kuripotiwa popote, huku wakazi na majirani wa nyumba hiyo wakisikia akikohoa na kulia usiku, na baba yake mzazi akiendelea na maisha kwa kumuogopa mkewe.



Wakizungumza na mwandishi jana, majirani hao walidai Mariam alihamia katika nyumba hiyo mwaka 2010, lakini hawakuwahi kumuona akiwa na mtoto. 



Hata hivyo majirani hao walikiri kwamba walikuwa wakisikia mtoto akikohoa na kulia hasa nyakati za usiku, lakini walikuwa na wasiwasi kuwa huenda mtuhumiwa alikuwa mshirikina anayefuga watu waliouawa kishirikina au kwa jina lingine misukule.



Hatimaye juzi mateso ya mtoto huyo yalipungua, baada ya msamaria mmoja kupata taarifa sahihi, kwamba ndani ya nyumba hiyo kuna kiumbe asiye na hatia aliye katika mateso na kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo.


Zongo akiwa katika kazi za kawaida katika mtaa huo, alipata taarifa kutoka kwa majirani kuwa kuna mwanamke, Mariam Said, amemficha mtoto ndani ya boksi na hamfanyii usafi wala kumtoa nje.


Akiwa Hospitali baada ya kuoshwa.
Baada ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta mwenyeji wake, Mwenyekiti wa mtaa huo, Tatu Mgagalana na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo ambapo walimkuta mtuhumiwa, Mariam na kuanza kumhoji kuhusu tuhuma hizo.


Kwa mujibu wa Zongo, wakati mtuhumiwa akijibu maswali aliyoulizwa huku akibabaika, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa hali iliyowapa wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa Mariam kwa nguvu, hatua iliyomuokoa mtoto huyo kutoka katika mateso ya zaidi ya miaka mitatu.


Ofisa huyo na mwenyeji wake walimkuta mtoto huyo ametapakaa uchafu uliotokana na kinyesi na mkojo, kwa kuwa boksi hilo lilikuwa chumba chake cha kulala, meza yake ya chakula na maji na choo kwa ajili ya haja ndogo na kubwa.


Hali ya mtoto huyo ilisababisha mashuhuda waliokuwa wamezunguka nyumba hiyo, kuanza kumshambulia Mariam kwa fimbo na mawe, na kumlazimu Zongo na mwenyeji wake kufanya kazi ya ziada kumnusuru mtuhumiwa kwa kutoa taarifa Polisi, huku wakijaribu kuzuia asidhurike.


Baada ya muda askari Polisi walifika na kumchukua mtuhumiwa na alipofika kituoni, inadaiwa alikiri kuanza kumlea mtoto huyo tangu akiwa na miezi tisa baada ya mama yake, kufariki dunia mwaka 2010.


Mtuhumiwa huyo alidai Polisi kuwa kwa mara ya mwisho, alimuogesha mtoto huyo Julai mwaka jana, na alikuwa akimwekea chakula na maji ndani ya boksi hilo.


Mume wa mtuhumiwa huyo, Mtonga Ramadhani ambaye ni mfanyabiashara wa Soko la Mawenzi katika Manispaa ya Morogoro naye alikamatwa na katika mahojiano, alidai hakuona sababu ya kutoa taarifa za kufichwa kwa mtoto huyo kwa sababu hamhusu na wajibu wake ilikuwa kutafuta chakula tu.


Kwa sasa mtuhumiwa huyo yupo Kituo Kikuu cha Polisi mjini Morogoro na mtoto amepelekwa katika Ofisi ya Idara ya Ustawi wa Jamii.
 




Baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alidai baada ya mzazi mwenzake kufariki dunia, alishindwa kumchukua mtoto wake kwa sababu tayari alishakuwa na mke. 


Alidai kwa kuwa alikuwa ameoa, alikubaliana na upande wa pili wa familia ya marehemu, kuwa mwanawe huyo alelewe na mama yake mkubwa, Mariam. 

 
Akizungumzia ulemavu wa mtoto huyo, Ofisa Ustawi wa Jamii, Oswin Ngungamtitu alisema ulemavu huo huenda umetokana na kuishi kwenye boksi tangu akiwa na miezi tisa hadi sasa bila kutolewa nje, kufanyiwa usafi wala kupewa chanjo mbalimbali ikiwemo ya polio.


Ngungamtitu alisema ulemavu huo pia huenda umetokana na kukosa lishe yakiwemo maziwa ya mama, hewa safi na upendo na kwamba mtoto huyo atakuwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo minyoo, nimonia, utapiamlo na malaria. 


Kutokana na hali hiyo, Ngungamtitu alisema ofisi yake imempeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ili akafanyiwe uchunguzi na kupewa chanjo ya kutibu magonjwa yatakayobainika.


Baada ya hapo kwa mujibu wa Ofisa huyo, mtoto huyo atapelekwa kwenye kituo cha kulelea watoto yatima na ikibidi atakabidhiwa kwa baba yake mzazi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, mwanamke huyo pamoja na mumewe wanashikiliwa Polisi kwa kosa la kumfanyia ukatili mtoto kinyume cha Sheria ya Mtoto ya 2009.

Post a Comment

 
Top