Watu watatu wafariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa katika matukio tofauti tofauti mkoani Iringa likiwemo la abiria mmoja wa IT aliyejulikana kwa jina la Sandes Kazeze (22) mkazi wa Malawi kufariki dunia baada ya gari alilokuwa amepanda kuligonga loli.
 
Akiwa ofisini kwake Kamanda wa polisi mkoani Iringa ACP Ramadhani Mungi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 28 mei majira ya saa 12 za Alfajiri huko katika Kijiji cha Iramba barabara kuu ya Iringa – Mbeya wilaya ya Mufindi.
Kamanda Mungi alisema marehemu alikuwa amepanda gari aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili IT 0116 mali ya Davious Timeson wa Malawi lililokuwa likiendeshwa na Madilisto Tambala (34) aliigonga gari aina ya scania lenye namba za usajili T 181 ARC likiwa na Trella namba T 972 AGR mali ya Mikoani Traders iliyoko Dar Es Salaam iliyokuwa ikiendeshwa na Edwin Komba (29) mkazi wa Dar Es Salaam na kusababisha kifo cha abiria mmoja na wengine wawili kujeruhiwa.
Kamanda aliwataja majeruhi hao ni Madilisto Tambala pamoja na Peter Malunda wote ni wakazi wa Malawi ambao kwa sasa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Ilembula na kusema chanzo cha tukio hilo ni mwendo kasi wa dereva.
Wakati huohuo, huko katika maeneo ya Mlima Chanagarawe barabara kuu ya Iringa – Mbeya wilayani Mufindi gari aina ya Mitsubishi Fuso yenye namba za usajili T 167 AVE mali ya Safina wa Makambako iliyokuwa ikiendeshwa na Jailet Kimbe (25) akitokea Dar es Salaam kuelekea 
Makambako aligongana na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 849 CHP lenye trella namba T 984 CNE mali ya Super star wa Dar es Salaam lililokuwa likiendeshwa na Hamad Mkubwa (47) na pia kuligonga gari jingine aina ya Scania lenye namba za usajili T 612 ASF lenye trella namba T 120 AFT mali ya Eawadhi kisha kuacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha tingo wa Mitsubishi Fuso aliyetambulika kwa jina la Noel Nyika (22) mkazi wa makambako.
Na katika tukio lingine, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Simon Mlomo (80) mahabusu na mkazi wa Nyololo mwenye CC namba 20/2013 aliyekuwa anakabiliwa na tuhuma za mauaji amefariki dunia wakati akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Mufindi mkoani Iringa.
Mbali na matukio hayo ya vifo, Kamanda alisema watu wasiofahamika waliiba gari aina ya Toyota Carina yenye namba za usajili T 794 AYN lenye rangi nyeupe na thamani ya shilingi 6,000,000/= ambayo ni mali ya Edward Lucas (43) mkazi wa Kihesa.
Tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 28 mei na kusema gari hilo lilikutwa maeneo ya Mshindo likiwa limetelekezwa.
By. Francis Godwin.blogspot.com

Post a Comment

 
Top