PAMOJA na kuwa mmoja
kati ya mikoa 12 nchini iliyopewa kipaumbele katika kampeni ya tohara kwa wanaume,
mkoa wa Njombe unaelezwa kuwa na idadi kubwa ya wanaume ambao hawajatahiriwa.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya
hiyo, Sarah Dumba, hali hiyo inachangia mkoa huo kuwa kinara wa maambukizi ya
virusi vya Ukimwi (VVU) nchini.
Takwimu za kitaifa
zinaonesha mkoa huo ukiongoza kwa kuwa na asilimia 14.8 ya maaambukizi ya VVU,
ukifuatiwa na mkoa wa Iringa wenye asilimia 9.1.
Katika kukabiliana na
maambukizi hayo, moja ya mikakati iliyowekwa na mkoa huo ni kuwafikia na
kuwatahiri wanaume 91,156 kupitia kampeni hiyo inayoendelea.
Katika uzinduzi wa
kampeni ya upimaji wa VVU kwa hiari uliofanyika hivikaribuni katika kata
ya Lupemba, Dumba aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Kapteni Msaafu Aseri
Msangi alisema ongezeko la vifo na watoto yatima mkoani humo vimechangiwa na
ugonjwa wa Ukimwi ambao chanzo chake ni maambukizi ya VVU.
“Mpaka sasa mkoa na
wilaya zake zote unakadiriwa kuwa na watoto yatima zaidi ya 7,900 kati yao wa kike wapo zaidi ya 3,570;
takwimu hizi ni za juu mno kwahiyo ni muhimu tuepukana na yale yote
yanayochangia maambukizi hayo,” alisema.
Alisema mkoa wa Njombe una jumla ya vituo 88 vinavyotoa huduma ya upimaji VVU ka hiari na kwamba katika kipindi cha kati Julai 2013 hadi Machi 2014, jumla ya watu 22,681 walijitokeza kupima afya zao na kati yao 3,409 sawa na asilimia 15 walikutwa na maambukizi ya VVU.
Ili kufikisha huduma ya upimaji kwa watu wengi zaidi, alisema mkoa utaongeza vituo vya upimaji kutoka 88 vya sasa hadi 138.
Kwa Upande wake, Meneja wa shirika la Population Services International (PSI) wa Mikoa ya Njombe na Ruvuma, Wilfred Lukungilwa aliwasihi wananchi wa mkoa huo kuendelea kutumia kondomu kama moja ya kinga dhidi ya maambukizi ya VVU.
Post a Comment