Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombea akikagua zahanati ya Mlangali baada ya kuifungua na kugundua vifaa alivyovinunua ili viletwe hapo kwa matumizi ya wagonjwa havikuletwa.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe akiwahoji kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ludewa Bw.Horace Kolimba wa katikati  na kaimu mganga mkuu wa Wilaya  ya Ludewa.
Filikunjombe akionyesha moja ya chombo  cha  kuhifadhia  dawa  za  chanjo ambacho ni pekee kilicholetwa katika zahanati hiyo wakati vilitakiwa kuwapo vinne.

Wananchi  kijiji cha Mlangali wilayani Ludewa  wakimpongeza Mbunge wao kwa  kuwatimua  wakuu wa Idara za halmashauri ya wilaya ya Ludewa mkutanoni
Mbunge  wa  jimbo la  Ludewa  Deo  Filikunjombe  amewatimua katika mkutano  wa hadhara wakuu wa  idara sita  akiwemo kaimu mkurugenzi wa  Halmashauri ya  wilaya ya  Ludewa  Horace Kolimba  kutokana uzembe  wa  kushindwa kupeleka  vitanda katika  Zahanati  hiyo  kwa  mwaka mmoja  sasa mbali ya  vitanda  hivyo kuvinunua kwa  pesa  zake na kutoa fedha ya kuvisafirisha.

Hatua  hiyo  imekuja  muda mufupi  baada ya  mbunge  huyo kufungua  rasmi zahanati  hiyo na  kukutana na changamoto ya  vitanda pamoja na nyingine  nyingi ambazo  zimesababishwa na uzembe wa mkurugenzi  mtendaji wa Halmashauri ya  Ludewa Wiliam Waziri ambaye muda mwingi anadaiwa kuutumia kwaajili ya safari mbalimbali akiacha kutekeleza majukumu yake ofisini.


Tukio  hilo  limetokea  jana  mchana katika  kijiji cha Mlangali  ndani  wakati  wa  uzinduzi  wa Zahanati  hiyo huku  wananchi  waliokuwepo katika mkutano  huo  wakiwazomea na baadhi  yao  walimweleza Mbunge kuwa halmashauri hiyo inakabiliwa na tatizo la ufisadi katika kila Idara.
 
Filikunjombe alisema Serikali ya awamu ya Nne inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete imekuwa ikiwajali wananchi kufanya mambo mbalimbali lakini tatizo liko kwa vingozi wa ngazi za chini ambazo zimekuwa zikikwamisha maendeleo kwa wananchi bila sababu za msingi.
 
Alisema hata kubali hata siku moja kuona wananchi wakinyanyasika kwa kukosa huduma muhimu kwa uzembe wa watendaji wa Serikali ambao wanashindwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ikiwa chama hicho kinawajali na kuwathamini wananchi ambao ndio walioiweka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania madarakani.

Kabla ya  kuwatimua  wakuu  hao wa idara mbao  walikuwepo katika msafara huo mbunge  Filikunjombe aliwaweka kitimoto  kaimu mganga mkuu wa  wilaya ya Ludewa  Godlove Katemba na kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya  wilaya ya Ludewa Horace Kolimba ili kueleza  sababu ya kushindwa  kupeleka vitanda katika zahanati  hiyo kwa muda wote  huku  kiasi cha zaidi ya Tsh milioni 5 alitoa  kwa mkurugenzi .

Akieleza sababu  za kuchelewa kufika kwa vitanda  hivyo kaimu mganga mkuu Godlove alisema kuwa ni kutokana na Halmashauri  hiyo kukosa fedha  za  mafuta   lita  20  kwa ajili ya kujaza katika gari  ambalo  lingesafirisha  vitanda  hivyo.

" Samahani  mheshimiwa  kweli  vitanda  tulivipata  kutoka  ofisi yake kwa ajili ya  Zahanati hii Mlangali  ila tumeshindwa  kuvileta kwa wakati kutokana na kukosa mafuta ila  ndani ya  wiki moja  vitakuwa  vimefika haopa"

Wakati  kaimu mkurugenzi  huyo Bw Kolimba  alikiri  kuwepo kwa uzembe na kuomba kulishughulikia  suala  hilo haraka  iwezekanavyo .

Majibu ya   kujichanganya na  kuonyesha  kutojua  chochote  juu ya kuchelewa  kufika kwa vitanda  hivyo yalipelekea  mbunge  huyo  kuwaita mbele  wakuu  wote  sita  wa idara  ambao  walikuwepo meza  kuu na kuwataka  kuondoka mkutanoni hapo kwenda  Ludewa  kufuata  vitanda  hivyo na kupingana na  maombi ya kaumi mganga mkuu aliyeomba  kuvipeleka  vitanda  hivyo ndani ya wiki mmoja .

" Hebu naomba watumishi  mnijibu kuna  mwezi hata mmoja serikali  imeshindwa  kuwalipa mishahara  yenu,sasa  kwa  nini mmekuwa  mnawafanyia  hivyo   wananchi hivi tujiulize  Halmashauri  imeshindwa  kupata  lita  40  za mafuta ambazo ni  chini ya Tsh 50,000 mbona  fedha  ya  kwenda  semina  yenye  posha kwa  wakuu wa idara zipo siwezi  kuwaacha kwa  uzembe  huu  wote  simameni ondokeni  mrudi wilayani mkalete vitanda hivyo  leo na  mimi nawasubiri hapa na  wananchi "

 Filikunjombe alisema  kuwa  siku  zote  watendaji  wabovu  serikalini  ndio ambao wamekuwa  wakipelekea  wananchi kuichukia serikali   na  chama  tawala wakati  uzembe  umekuwa  ukifanywa na baadhi  ya  watumishi  wachache  wa  serikali.

" Hivi  wananchi nawaulize katika hili  la  vitanda hapa ni nani  wa kulaumiwa kama  mimi  mbunge  nimetoa vitanda  hivyo  toka mwaka jana tena pamoja na  pesa ya  kusafilishia hadi hapa ila  wao  wameendelea  kuvihifadhi stoo na  wagonjwa  wakiendelea  kulala  chini ardhini ....hapana  nasema  mimi bado  naupenda  ubunge na sipo tayari  kutolewa madarakani kwa  uzembe kama huu hivyo nasema wataanza  kutoka  wao kabla ya mimi kutolewa na wananchi "

Kwani  alisema  katika Zahanati  hiyo  yeye kama mbunge amepata kutoa msaada  wa vitanda  hivyo vinne  ,magodoro  yake  ,mashuka pamoja na gari  la wagonjwa ila ni vitu  vichache pekee ndivyo  amevikuta  hapo  likiwemo gari na mashuka  wakati magodoro hadi sasa hakuna .

Kufukuzwa  kwa aibu  kwa  wakuu hao  wa  idara  mkutanoni kuliamsha  hasira  ya  wananchi  waliokuwepo mkutanoni hapo ambao  walishindwa  kujizuia  kuwazomea huku  baadhi yao  wakiwemo vijana  wakimwomba  mbunge  huyo awape  ruhusa ya  kuwasindikiza wakuu  hao wa  idara kwa fimbo kama  njia ya kuwakumbusha  wajibu  wao jambo ambalo mbunge alionyesha kupingana nalo kwa madai kuzomewa  kwao ni adhabu tosha.

Awali mganga  mkuu wa  Zahanati hiyo Prica Mgina  alimweleza  mbunge  huyo kuwa tatizo la Zanahati  hiyo ni kukosekana kwa  vitanda vya kulazia  wagonjwa na  kupelekea  wagonjwa  kulazwa  sakafuni  pia  firiji la kuhifadhia  dawa za  chanjo limekuwa likikaa bila  kutumika kwa mwaka mmoja sasa toka lifike hapo kutokana na trei mbili  kati ya nne za  kuhifadhia dawa kukosekana japo zipo Hospitali ya wilaya .

Wakuu  hao  wa  idara  waliofukuzwa katika mkutano huo ni pamoja na kaimu mkurugenzi Horace Kolimba , Kaimu mganga  mkuu wa  wilaya  Godlove Katemba ambae pia ni katibu wa afya  wilaya ,kaimu afisa  elimu Joseph  Mvanga ,kaimu afya kilimo na mifugo Betrice Bethod,kaimu muhandisi wa ujenzi Brait Komba  na kaimu muhandisi wa  idara ya maji Malicela Maisha .

Hata  hivyo mbali ya  awali  wakuu hao wa idara  kuomba  vitanda  hivyo kuvileta  ndani ya  wiki mmoja Zahanati hapo  bado  waliweza  kuvifikisha  vitanda hivyo ndani ya masaa 2 baada ya kwenda  makao makuu ya wilaya umbali wa km zaidi ya 50 na kuvisafirisha  vitanda  hivyo kama walivyoagizwa na mbunge Filikunjombe.

Diwani wa kata  hiyo ya Mlangali Faraja  Mlelwa (chadema) alimpongeza  mbunge  huyo kwa kuwatumikia wana Ludewa kwa vitendo na  kumtaja  kuwa ni mmoja kati ya  wabunge  wachache ambao wamekuwa  wakiwatumikia kwa vitendo  wananchi hao hivyo  kuahidi kuonyesha  ushirikiano  zaidi kwa  mbunge  huyo huku akiwataka  wananchi  kuweka kando itikadi  vya vyama  vyao na kushiriki maendeleo

Post a Comment

 
Top