Deni la Sh 2,000 limetosha kumaliza uhai
wa mpiga debe maarufu wa stendi ya mabasi yaendeayo mikoani ya mjini
Iringa, Samwel Yengayenga baada ya kuchomwa kisu mara mbili katika eneo la mgongoni
na kifuani.
Tukio hilo la kinyama limetokea leo
majira ya saa 6.55 mchana baada ya Yengayenga na mtuhumiwa wa mauaji yake
aliyekuwa akidai kiasi hicho cha fedha kurushiana maneno makali na kisha
kupigana.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni
Festo Ruben Mkalala (26), muosha magari, mkazi wa mjini Iringa ambaye
alikamatwa mara baada ya kufanya tukio hilo.
Mungi alisema Yengayenga, Mkalala na mtu
mwingine wa tatu (hakumtaja jina) wanadaiwa siku nne zilizopita waliosha basi
la Kimotco linalofanya safari zake kati ya Iringa na Arusha.
“Stahiki ya kazi hiyo ilikuwa Sh 15,000;
hata hivyo hawakulipwa fedha hizo baada ya kumaliza kazi hiyo,” alisema.
Alisema siku iliyofuata Mkalala na kijana
huyo mwingine waliyefanya naye kazi walikwenda kuchukua ujira wao na kugawana
Sh 5,000 kila mmoja huku Mkalala akiahidi kutunza Sh 5,000 za Yengayenga mpaka
watakapokutana.
Walipokuta, RPC alisema Mkalala alimpa Yengayenga
Sh 3,000 badala ya Sh 5,000 na kuahidi kummalizia kiasi kilichobaki kesho yake.
Kitendo hicho kwa mujibu wa mashuhuda
kinadaiwa kumchukiza Yengayenga aliyeamua kunyanganya simu ya Mkalala mpaka
amaliziwe Sh2,000 zake zilizobaki.
Kamanda Mungi alisema Mkalala alichukizwa
na uamuzi huo na kuanzisha ugomvi uliopeleka kifo cha Yengayenga.
“Uchunguzi wa awali unaonesha Mkalala
aliamua kupigana na Yengayenga ili arudishiwe simu yake na alipozidiwa
alikimbia kusikojulikana na kurudi akiwa na kisu mkononi,” alisema.
Ili kuipata simu yake, Kamanda Mungi
alisema ushahidi wa awali unaonesha Mkalala alitumia kisu hicho kumchoma
mgongoni na kifuani Yengayenga na kusababisha mauti yake.
Yengayenga alikufa papo hapo katika tukio
ambalo mtuhumiwa huyo alikamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi cha kati cha
mjini Iringa.
Post a Comment